WAZIRI WA MADINI ALITAKA SHIRIKA LA MAENDELEO LA TAIFA (NDC) KUVITAMBUA VIPAJI NA UWEZO WAANZILISHI WA VIWANDA ILI KUWAJENGEA UWEZO | ZamotoHabari.

Waziri wa Madini Dotto Biteko amelitaka shirika la maendeleo la taifa (NDC)kujipa muda wa kuvitambua vipaji na uwezo walionao waanzilishi mbalimbali wa viwanda na kuona wanawasaidiaje katika kukuza uwezo wao badala ya kukimbilia kuulizia vibali au leseni ya shughuli zao.

Biteko ameyasema hayo alipotembelea kiwanda kidogo cha kulainisha chuma kilichopo katika kata ya Lubonde wilaya ya Ludewa mkoani Njombe kinachomilikiwa na Bw. Reuben Mtitu (Mzee Kisangani) na kuona uwezo wake katika kutengeza vitu mbalimbali vya chuma ikiwemo visu,ma panga, nyundo, mafyekeo n.k, huku changamato yake kubwa ikiwa ni rasilimali za uzalishaji wa bidhaa zake.

Alisema serikali inapaswa kutambua kuwa kwa sasa teknolojia inakuwa hivyo si vyema kuwapa kipaumbele watu kutoka nchi za nje badala yake ianze kusaidia watu wenye teknolojia mbalimbali waliomo ndani ya nchi na kuwasidia kukuza teknolojia hiyo na si kuwawekea vizuizi.

Aliongeza kuwa katika halmashauri ya Ludewa kuna makaa ya mawe mengi sana lakini inashangaza kuona Bw. Mtitu anashindwa kupata makaa hayo kwa ajili ya kulainishia chuma kwa sababu sheria zilizopo zinamkataza kuchimba makaa hayo kitu ambacho kinarudisha nyuma uzalishaji wake na kushindwa kukua kwa kiwanda hicho.

“Tatizo letu watanzania tunapenda kuhangaika na madhaifu ya watu badala ya kuangalia nini alichonacho mtu na kukipa sapoti kitu ambacho kinafanya tushindwe kuendelea kwa kisingizio cha kufuata sheria, hizi sheria zipo kwa ajili yetu na si kwamba sisi tupo kwa ajili ya sheri hivyo mzee huyu kwakuwa ameonyesha uthubutu awe na leseni au la! ni lazima awekewe utaratibu wa kupata makaa hayo ili kiwanda chake kiweze kukuwa”, alisema Biteko.

Alisema ili kuunga mkono sera ya Mh. Rais Joseph Pombe Magufuli juu ya viwanda atakaa kikao na NDC pamoja na uongozi wa mkoa wa Njombe ili kuona ni jinsi gani wanaweza kuwasaidia wachimbaji wadogo wa makaa ya mawe kupata lesenia ili kama kuna sheria inazui wachimbachi hao kuchimba ni lazima tufanye haraka kuirekebisha ili kukuza teknolojia hizo na kuongeza pato la nchi.

Aidha kwa upande wa Bw. Mtitu alisema kuwa kwa sasa yupo katika majaribio ya uyeyushaji huo na anakabiliwa na tatizo kubwa la upatikanaji wa makaa ya mawe na kupelekea kuvizia magari yaliyobeba makaa ya hayo kutoka Songea yanapodondoka ndipo aweze kuokota na kuja kufanyia kazi katika kiwanda chake.

Pamoja na changamoto hiyo ya makaa ya mawe pia hana jengo la kufanyia shughuli zake kitu ambacho kinamlazimu kufanya shughuli zake kwa msimu wa kiangazi tuu badala ya kufanya kwa kipindi chote cha mwaka mzima, mtaji wa kuendeshea utafiti wao pamoja na malighafi.

Alisema kuwa ujio wa waziri umempa matumaini makubwa sana kwakuwa ameahidi kumsaidia katika changamoto zake kubwa zinazomkabili hivyo itamsaidia kuzalisha vitu vingi zaidi kwani anampango wa kuzalisha chuma kwa wingi kwa ajili ya bidhaa zake na kuwauzi wenye viwanda vikubwa vya nondo kwakuwa chuma kinachopatikana wilayani humo ni bora zaidi. 
 Waziri wa madini Dotto Biteko akiangalia mashine ya kuyeyusha chuma ambayo ni hatua ya awali katika kiwanda kidogo cha kuyeyusha chuma kilichopo wilayani Ludewa mkoani Njombe
 Waziri wa madini Dotto Biteko akiangalia kinu cha kuyeyusha chuma katika kiwanda kidogo cha kuyeyusha chuma kilichopo wilayani Ludewa mkoani Njombe.
 Mmiliki wa kiwanda kidogo cha kuyesha chuma Bw. Reuben Mtitu (Kisangani) kilichopo wilaya ya Ludewa mkoani Njombe
Mkuu wa wilaya ya Ludewa Andrea Tsere, akiteta jambo na waziri wa madini Dotto Biteko walipotembelea kiwanda kidogo cha kuyeyusha chuma kilichopo wilaya ya Ludewa mkoani Njombe


APP YETU MPYA: Sasa unaweza kusoma kwa urahisi kupitia APP yetu. Download hapa kwa KUBOFYA HAPA

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini