JARIBU kufikiria upo kwenye ndoa kwa muda wa miaka 20 au zaidi, ndoa yenu ikiwa imebarikiwa kuwa na watoto watatu, ghafla unapata habari za uhakika na zenye uthibitisho rasmi kuwa kumbe hao watoto wote ambao unaona ni wa kwako, siyo hivyo, yaani siyo damu yako!
Hisia ambazo utazisikia au unahisi kuwa unaweza kuzihisi mara baada ya kupata jibu la hilo ambalo umelisoma hapo juu, ndicho kitu ambacho kiliwahi kumtokea straika wa zamani wa Ghana na timu kadhaa kubwa Ulaya, Nii Odartey Lamptey.
Jina la mshambuliaji huyu ambaye kwa sasa umri wake ni miaka 45, limerejea kwenye vyombo vya habari baada ya kesi yake na aliyekuwa mkewe huyo ambaye ‘alimbambikia’ watoto watatu kutolewa maamuzi na mwanaume huyo kushinda.
Kesi hiyo ilikuwa kuhusu mjengo wa thamani ambao mkewe huyo wa zamani, Gloria Appiah alikuwa akiishi mara baada ya wawili hao kutalikiana.
Lamptey alipeleka kesi mahakamani akitaka mwanamke huyo aachie jumba hilo lililopo East Legon na mahakama imetoa amri kuwa Gloria anatakiwa kuondoka haraka kwa kuwa hana mamlaka ya umiliki wa mjengo huo.
Awali alishindwa lakini akakata rufaa na sasa ameshindwa tena, hivyo nyota huyo wa zamani wa timu ya taifa ya Ghana ‘Black Stars’ pamoja na timu za Anderlecht ya Ubelgiji, PSV (Uholanzi), Aston Villa na Coventry City zote za England, ana haki ya kufanya anachotaka kwenye nyumba hiyo.
Majaji watatu waliosikiliza rufaa hiyo wameagiza jumba hilo lenye vyumba saba vya kulala na vitu vingine vingi vya thamani, sasa ni mali halali ya Lamptey ambaye kwa sasa ni kocha wa soka.
Filamu ilivyoanza
Wawili hao walitalikiana mwaka 2013. Lakini sababu ya safari yao kuelekea kwenye mvurugano inasikitisha na inashangaza.
Baada ya kucheza soka kwa muda mrefu katika mataifa tofauti, ndoa yao ikiwa na miaka 20, alistaafu na kutokuwa na kipato kikubwa kama alichokuwa akikipata awali.
Hapo mambo yalianza kuvurugika kiasi, migogoro ikaanza kuibuka mara kwa mara.
Ugomvi wa kutolipa ada
“Ilianza kama utani, tulivurugana baada ya mimi kushindwa kulipa ada ya watoto ambayo kwa wakati huo ilikuwa ni gharama kubwa sana.
“Alitaka watoto wasome Uingereza na ada yao ilikuwa pauni 26,000 (Sh milioni 75.7). Niliona baada ya kucheza soka nimekusanya fedha zangu kisha zote ziishie kwenye kuwalipia ada watoto siyo sawa. Hiyo ni kwa kuwa watoto wote watatu walitakiwa kulipiwa ada hiyo kila mmoja.
“Maamuzi niliyoamua ni kuwatafutia shule ya gharama nafuu, hapo ndipo ugomvi ukaanzia,” anasema Mghana huyo.
Baadaye familia ikawa haina amani ndani na akaanza kusikia tetesi kuwa mkewe hakuwa mwaminifu, mke huyo akaanza kudai talaka kwa kuwa hawakuwa na maelewano mazuri ndani kisa kikiwa ni ada.
Lamptey anasema watu wake wa karibu wakaanza kumwambia kuwa wana wasiwasi kuwa inawezekana hata hao watoto aliozaa na mwanamke huyo siyo kwa kwake kwa kuwa mkewe hakuwa na nyendo nzuri.
Hivyo, wakamshauri akapime vinasaba (DNA) vya watoto kupata uhakika juu ya suala hilo.
Wakati huo mkewe alikuwa akisisitiza kutaka talaka kisha wagawane mali walizochuma wakiwa pamoja asilimia 50 kwa 50.
“Watoto wakati huo walikuwa na umri wa miaka 18, 19 na 20 kitu kama hicho. Ukweli ni kuwa ulikuwa wakati mgumu sana kwangu.
“Watu wengi wakawa wananipigia simu kuniambia kuhusu watoto wangu, wengine wananishauri hivi mara vile. Ikanibidi nianze kufanya uchunguzi wa kina, nilikuwa kama mpelelezi.
“Wengine wakanishauri nikapime DNA, nilipoambiwa hivyo ilinishtua sana, kwa kuwa mwanamke tayari alikuwa ameshafungua kesi mahakamani akidai talaka.
“Sikuwa najua chochote kuhusu mambo ya DNA, ikanibidi nizungumze na mwanasheria wangu kuhusu suala hilo, naye akanipa muongozo mzuri wa nini natakiwa kukifanya. Alikubali kuwa natakiwa kwenda kupima DNA na watoto hao ambao walikuwa ni mabinti.
Awadanganya watoto kupima DNA
“Kwa kuwa kesi ilikuwa mahakamani hata watoto sikuwa nao karibu kama ilivyokuwa mwanzo, nikaamua kufanya mbinu ya udanganyifu ili kukamilisha kile nilichokipanga.
“Nilimchukua daktari binafsi, nikaenda hadi chuoni kwao nikaonana nao, niliwaambia nimefika pale kwa ajili ya kuwalipia ada na kuwapa hela ya matumizi, pia kuna suala la kiafya ambalo walitakiwa kushughulikiwa.
“Nikawaambia kuwa imebainika nina matatizo kwenye koo langu, na ninapatiwa matibabu, daktari kaniambia watoto wangu pia wanatakiwa kuchunguzwa ili isije kuwatokea tatizo kama la kwangu kwa kuwa linaambukizwa, hivyo wanatakiwa kupatia tiba mapema.
“Nikawaambia nimekuja na daktari ambaye anatakiwa kuwafanyia uchunguzi ili kama tatizo lipo waliwahi mapema.
“Wakakubali, wakachukuliwa mate yao kupitia vifaa maalum na vingine ambavyo daktari alikuwa akihitaji kutoka kwao, wote watatu.
“Majibu yalitakiwa kutoka baada ya wiki mbili, lakini kwa kuwa kulikuwa na kesi mahakamani, daktari akaniambia kuwa itachukua mwezi mmoja ili wao wapate jibu la uhakika kabisa wasije wakatoa majibu yenye utata.
“Siku naenda kuchukua matokeo, nikakutana na daktari akaniuliza ‘Una muda gani kwenye ndoa hii’, nikamwambia ‘miaka 20’, wala hakung’ata maneno akaniambia moja kwa moja ‘hawa watoto siyo wa kwako’.
“Unaweza kupata picha majibu hayo jinsi ambavyo niliyapokea, nilipata mtikisiko na mshtuko mkubwa sana, kumbuka pia wakati nafanya masuala ya DNA sikumwambia mke wangu wala watoto.
“Nilipigwa ganzi kama dakika mbili hivi baada ya majibu hayo kisha nikampigia simu wakili wangu na kumwambia kuhusu majibu hayo.
“Akaniambia nimfuate alipo, nikamwambia siwezi kuendesha gari kwa muda huo, ikabidi anifuate na akasema tutatumia ushahidi huo kwenye kesi ya talaka iliyokuwa mahakamani.
“Nilikuwa na huzuni kubwa, nilijihisi kuwa mnyonge muda wote. Wakaanza kusema kuwa sina uwezo wa kumpa mwanamke ujauzito, iliniumiza sana.”
Avurugwa aamua kujiongeza
Baada ya kuona ndoa yake imeshavunjika, aliamua kuendelea na maisha yake huku kesi ya masuala ya mali ikiwa bado mahakamani.
Apata kimwana mpya
Akiwa bado kwenye msongo wa mawazo na maisha ya unyonge, alikutana na mwanadada Ruweida Yakubu ambaye ni staa wa filamu nchini Ghana.
Anasema: “Namshukuru sana Ruweida, kwanza alinikuta nikiwa katika hali mbaya kisaikolojia, nikaanzisha uhusiano naye lakini sikuwa sawa, alipambana kuniweka sawa na kunipa furaha.
“Miezi sita baada ya uhusiano wetu akaniambia amepata ujauzito, kwanza sikuamini (anasita, anatafakari kwa sekunde kadhaa).
“(Kabla hajaendelea, machozi yanamtoka) Kuna wakati ilifika nikataka kujiua, kuna wakati nilitaka nifungulie mashtaka wale wote waliokuwa wakiandika au kuripoti habari zangu.”
Aamua kuhama nyumba
“Wakati kesi ya mali ikiendelea na akiwa kwenye uhusiano wake mpya, wakili wangu alinishauri nihame pale nyumbani kwa kuwa chochote kinaweza kutokea, labda kauli au matendo yanaweza kunikera hivyo kusababisha mambo mengine ambayo hayatakiwi, hivyo akaenda kuishi hotelini.
Kuhusu wale watoto watatu
“Ukweli ni kuwa sina tatizo nao hata kidogo, wao hawana hatia yoyote kuhusu hiki kinachoendelea, walijua mimi ndiyo baba yao, niliwaacha wakaendelea na maisha yao.
“Nashauri tu wanaume wenzangu kuwa ni vema inapotokea wenza wao wamejifungua wakapata uhakika juu ya watoto wao, kulea watoto kwa miaka yote hiyo kisha unakuja kuambiwa siyo wa kwako ni darasa kubwa japo sijakaa darasani.”
Alipoulizwa kama anawasiliana nao au anaonana mara kwa mara mabinti hao watatu anasema: “Hapana, sijaonana nao wala siwasiliani nao, nilishauriwa iwe hivyo kwa kuwa lolote linaweza kutokea, mfano naweza kuzungumza kitu ambacho siyo kwa nia mbaya lakini wakakichukua tofauti na kunishitaki.
“Kitu pekee ambacho ni zawadi yangu kwao ni elimu nzuri niliyowapa kwa gharama kubwa.
Maisha ya sasa
“Nimepoteza mali na vitu vingi sababu ya kesi hiyo lakini kwangu vyote hivyo si kitu kwa kuwa maumivu niliyoyapata yalikuwa makubwa kuliko mali.”
“Sasa ninaishi maisha ya furaha, nina familia nzuri, mabinti zangu mapacha kila ninapowatazama wananipa furaha na wanani…..(anatoa machozi).
“Nashukuru Mungu naendelea vizuri, labda ningekuwa nimeshazikwa na kusahaulika kwa sasa kwa kilichonitokea. Nashukuru nina akademi ambayo inaendelea vizuri na inaibua vipaji vingi vya soka.
“Mahakama imerejesha nyumba yangu na sasaa nitaendelea vizuri na maisha yangu kama kawaida.”
Lamptey anaishi na Ruweida ambaye ndiye mama wa watoto wake halali wawili mapacha ambao bila hata DNA wamefanana na baba yao kwa kiwango cha juu.
Ushauri kwa wachezaji
Enzi zake Lamptey alikuwa nyota mkubwa, aliingiza fedha nyingi kupitia mchezo wa soka anatoa ushauri kwa wachezaji wenzake:
“Ni vema kujifunza kuchagua mtu sahihi kwa ajili ya maisha yako kitu ambacho ni kigumu kwa kuwa ukiwa maarufu kila msichana atataka kuwa mkeo. Kuna vishawishi vingi sana.
Kuhusu nyumba yake
“Nashukuru imerejea kwenye mikono yangu, bado sijaamua nini cha kufanya kama nirejee niishi hapo au nipangishe au niiuze, nimepata maoni mengi sana, bado sijaamua nini nitakifanya kuhusu nyumba hiyo.
Ikitokea akakutana na mke wa zamani
“Sina cha kumfanya lakini labda naweza kumuuliza swali moja tu kuwa ‘nilifanya nini hadi nikastahili mateso kama yale aliyonipa wakati nilimpa kila kitu?’.
Mtoto wa tatu yupo njiani
Lamptey anafichua kuwa mkewe mpya ni mjamzito. “Nimeamua twende mbio kidogo ili watoto wangu wapate elimu nzuri nikiwa bado nina nguvu, kwa sasa mke wangu ana ujauzito na anaendelea vizuri. Pia ni kwa kuwa umri haupo upande wangu, ndiyo maana imekuwa hivyo.
Makuzi yake
Lamptey alikulia katika familia yenye maisha ya kawaida, baba yake alikuwa mlevi na mara nyingi alimpa kipigo yeye Lamptey. Wazazi wake walitalikiana alipokuwa na umri wa miaka nane.
Mama yake alipoolewa na mwanaume mwingine, Lamptey akafukuzwa nyumbani na baba yake wa kambo. Akahamia kwenye kambi ya Waislamu waliokuwa wakicheza soka, huko alibadili dini kutoka kuwa Mkristo na kuwa muumini wa dini ya Kiislamu.
Huko ndiko alikoendelea kucheza soka na kuwa mkubwa, lakini mwaka 1997 alirejea kuwa Mkristo baada ya baba yake mzazi kujirudi na kuyamaliza.
Alistaafu kucheza soka la kulipwa mwaka 2008. Aliwahi kukorofishana na nguli wa soka wa Ghana, Abedi Pele, lakini haikuwahi kujulikana ugomvi wao ulihusu nini hasa.
Nii Lamptey
Kuzaliwa: Tema, Ghana
Urefu: Futi 5 inchi 7
Timu alizocheza
1990–1995 Anderlecht
1993–1994 → PSV (mkopo)
1994–1995 → Aston Villa (mkopo)
1995–1996 Coventry City
1996–1997 Venezia
1997 Unión Santa Fe
1997–1998 Ankaragücü
1998–1999 União Leiria
1999–2001 Greuther Fürth
2001–2002 Shandong Luneng
2003–2004 Al-Nasr Dubai
2005–2006 Asante Kotoko
2006–2008 Jomo Cosmos
Ghana
1991–1996
Mechi: 38
Mabao: 8.
JOHN JOSEPH NA MTANDAO
APP YETU MPYA: Sasa unaweza kusoma kwa urahisi kupitia APP yetu. Download hapa kwa
KUBOFYA HAPA
0 Comments