TIC YAANDIKA HISTORIA,YAFANIKIWA KUSAJILI MIRADI 1,312 YA UWEKEZAJI YENYE THAMANI YA TAKRIBANI SHILINGI TRILIONI 46 ZA KITANZANIA | ZamotoHabari.

Grace Semfuko, Dar es Salaam

Kituo cha Uwekezaji Tanzania-TIC katika kipindi cha Januari 2016 hadi Juni 2020 kimefanikiwa kusajili miradi 1,312 ya Uwekezaji yenye mtaji wa thamani ya Dola za Marekani Bilioni 20 ikiwa ni takribani Shilingi Trilioni 46 za Kitanzania, miradi hiyo inatoa ajira kwa watanzania 178,101.

Katika usajili huo Sekta ya usindikaji na uzalishaji wa Viwanda iliongoza kwa asilimia 54 ya miradi yote na kutoa ajira ya watanzania 67,992.

Akizungumza na Waandishi wa Habari Jijini Dar es Salaam kuhusu mafanikio ya Kituo cha Uwekezaji Tanzania katika kipindi cha miaka mitano madarakani ya Rais Dkt John Pombe Magufuli, Mkurugenzi wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania-TIC Bw. Geoffrey Mwambe amesema mafanikio hayo yanatokana na uongozi thabiti wa Serikali ya sasa.

"Katika awamu hii ya Magufuli, TIC imeendelea kutekeleza mpango mkakati wa miaka mitano, tulikuwa na Dira ya kufikia Kituo Bora kabisa Duniani kwa kuvutia Uwekezaji endelevu" alisema

Aliongeza kuwa Serikali ya Tanzania inao uwezo mkubwa sana wa kufanya maendeleo ya kasi na kwamba ndani ya miaka mitano tu hali ya uchumi na maendeleo ya Taifa yamebadilika kwa kiwango kikubwa kuliko ilivyotarajiwa.

*"Watanzania tunapaswa kujivunia, ndani ya miaka mitano tumebadili kabisa hali yetu ya uchumi na maendeleo ya Taifa yamekuwa kwa kasi sana, watu wengi wanaokuja hawaamini kuwa hii ni Tanzania, wanadhani ni ile Tanzania ya awali ambayo hatukuwa na uwezo wa kujenga miundombinu yetu wenyewe kama Reli ya kisasa ya Standard Gauge na mengineyo, wanabaki tu kuhoji Tanzania mnaweza? Na sisi tunasema ndio! Tunaweza" alisema Mwambe.

Alizungumzia pia uboreshwaji wa TIC kwenye eneo la huduma za mahala pamoja (One Stop Facilitation Centre) akisema zimeboreshwa na kuongezwa idadi ya Taasisi  zinazohudumia Wawekezaji kutoka Taasisi saba Mwaka 2015 na kufikia Taasisi kumi Mwaka 2020 huku idadi ya watumishi kwenye eneo hilo wakiongezeka kutoka 14 hadi 25.

Kuhusu kuongeza huduma za Uwekezaji kwenye maeneo yote nchini, Mwambe alisema Ofisi za  Kanda za TIC zimeongezeka kutoka Kanda tatu Mwaka 2015 hadi kufikia Saba Mwaka 2020 na kuzitaja Kanda hizo kuwa ni pamoja na Kanda ya Ziwa, Kanda ya Kati, Kanda ya Kusini, Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Kanda ya Kaskazini, Kanda ya Mashariki na Kanda ya Magharibi.

Aidha alizungumzia pia hatua ya TIC ya kuimarisha kamati ya Taifa ya uwezeshaji Uwekezaji (NIFC) ambayo inahusisha Wakuu wa Taasisi za Serikali zinazotoa vibali na  leseni mbalimbali za Uwekezaji yenye jukumu la kusaidia kuondokana na changamoto za Sekta hiyo kwenye maeneo yanayosimamiwa na Taasisi hizo.

Katika hatua nyingine Mwambe amesema TIC imeboresha mifumo ya kuchakata na kutoa vibali kwa njia   ya mtandao ikiwepo utoaji wa cheti cha vivutio, usajili wa kampuni pamoja na vibali vya kazi na ukaazi pamoja na kuwa na mkakati wa pamoja wa kushirikiana kwenye shughuli zote za uhamasishaji Uwekezaji na Biashara.

Mwambe hakuacha kuzungumzia tafiti zinazofanywa na Kituo hicho ambapo amesema ulifanyika Utafiti kuhusu mienendo ya mitaji ya Uwekezaji toka nje ili kubaini hali halisi ya ukuaji, fursa na changamoto za kisekta ili kuziboresha huku akizitaja tafiti hizo kuhusika kwenye maeneo ya Kilimo, Mifugo, Viwanda nq Mazingira ya Biashara kwa ujumla.

Katika mkutano huo na Waandishi wa Habari Jijini Dar es Salaam, Mwambe pia alitoa matokeo ya tafiti za athari za Uwekezaji zilizofanywa kufuatia kuibuka kwa ugonjwa wa Homa kali ya Mapafu- COVID-19 kwa Uwekezaji wa miradi iliyosajiliwa na TIC huku alitaja sekta ya Utalii na Viwanda vya uchakataji vinavyotegemea malighafi toka nje ya Nchi.

Alisema katika kipindi cha COVID-19  TIC iliendelea kufanya kazi kwa ustadi mkubwa na kuboresha mifumo ya utendaji kazi kwa kuzingatia ushauri wa wataalamu wa Sekta ya afya.

Mkurugenzi wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania(TIC), Geoffrey Mwambe akizungumza mbele ya Waandishi habari jana jijini Dar,alipokuwa akitoa taarifa ya mafanikio ya kituo hicho cha TIC katika kipindi cha miaka mitano ya Serikali ya awamu ya Tano.Mwambe alisema kuwa  katika kipindi cha Januari 2016 hadi Juni 2020 kimefanikiwa kusajili miradi 1,312 ya Uwekezaji yenye mtaji wa thamani ya Dola za Marekani Bilioni 20 ikiwa ni takribani Shilingi Trilioni 46 za Kitanzania, miradi hiyo inatoa ajira kwa watanzania 178,101.
 Baadhi ya viongozi Waandamizi wa TIC wakifuatilia yaliyokuwa yakielezwa na  Mkurugenzi wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania(TIC), Geoffrey Mwambe (hayupo pichani).
  Mkurugenzi wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania(TIC), Geoffrey Mwambe akizungumza mbele ya Waandishi habari jana jijini Dar,alipokuwa akitoa taarifa ya mafanikio ya kituo hicho cha TIC katika kipindi cha miaka mitano ya Serikali ya awamu ya Tano

  Baadhi ya Waandishi wa Habari na Viongozi waandamizi wa Kituo hicho wakimsikiliza  Mkurugenzi wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Geoffrey Mwambe alipokuwa akifafanua mambo mbalimbali ikiwemo mafaniko ya kituo hicho kwa miaka mitano ya Rais Dkt John Pombe Magufuli.
  Mkurugenzi wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania(TIC), Geoffrey Mwambe akionesha moja ya jarida linalochapishwa na kituo hicho,likieleza taarifa mbalimbali kuhusu mambo ya uwekezaji,mbele ya Waandishi wa Habari jana jijini Dar.Picha zote na Michuzi JR-MICHUZI MEDIA.


APP YETU MPYA: Sasa unaweza kusoma kwa urahisi kupitia APP yetu. Download hapa kwa KUBOFYA HAPA

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini