KISARAWE YAJIPANGA KUWAKABILI WATAKAOFANYA VURUGU, KUVURUGA AMANI KATIKA UCHAGUZI MKUU | ZamotoHabari.

 Mkuu wa wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani Jokate Mwegelo(katikati) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya maofisa wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania(JWTZ)akiwemo Mkuu wa Kikosi cha 191 Kisarawe Luteni Kanali Nichelewa, baada ya kufanyika kwa uzinduzi rasmi wa mafunzo ya jeshi la akiba (Mgambo) kwa vijana 150 wa wilaya hiyo.Mafunzo hayo yamefunguliwa leo Agosti 6,mwaka 2020.
 
Sehemu ya vijana wa Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani wapatao 150 wakiwa wamenyoosha mkono kama ishara ya kukubali maelekezo yaliyokuwa yakitolewa na Mkuu wa Wilaya hiyo Jokate Mwegelo wakati akizungumza nao alipokwenda kufungua rasmi mafunzo ya jeshi la akiba yaliyoandaliwa na wilaya hiyo.
 
Baadhi ya wanajeshi wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania(JWTZ) wakiwa kwenye ufunguzi wa mafunzo ya jeshi la akiba kwa vijana 150 wa Wilaya ya Kisarawe.Mafunzo hayo yamefunguliwa na Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe Jokate Mwegelo(hayupo pichani).
 
Jokate Mwegelo ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani akizungumza wakati akifungua mafunzo ya Jeshi la Akiba(mgambo)kwa vijana 150 wa wilaya hiyo ambapo amewasisitiza vijana hao kuwa wazalendo kwa nchi yetu.
 
Mshauri wa Jeshi la Akiba wilayani Kisarawe mkoani Pwani Meja  Mohamed Wawa(kushoto) akijadiliana jambo na Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe Jokate Mwegelo.
 
Mkuu wa Kikosi cha Mkuu wa Kikosi cha 191 Kisarawe Luteni Kanali Nichelewa akisalimiana na Mkuu wa wilaya ya Kisarawe Jokate Mwegelo baada ya kufunguliwa kwa mafunzo ya jeshi la akiba kwa vijana 150 wa wilaya hiyo.

 
Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe Jokate Mwegelo akiwa na maofisa wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania(JWTZ), Katibu Tawala wa Kisarawe Mwanana Msumi pamoja na vijana wanaopata mafunzo ya jeshi la akiba wakiwa katika dua maalumu baada ya kufunguliwa kwa mafunzo hayo.
 Mshauri wa Jeshi la Akiba wilayani Kisarawe Meja Mohamed Wawa akiwa katka dua na baadhi ya vijana wanaopatiwa mafunzo ya jeshi la akiba katika wilaya hiyo.
 Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani Jokate Mwegelo(kushoto) akiteta jambo na Katibu Tawala wa Wilaya hiyo Mwanana Msumi wakati wa uzinduzi wa mafunzo ya jeshi la akiba kwa vijana 150 wa wilaya hiyo.
Baadhi ya wananchi walioshiriki ufunguzi wa mafunzo ya jeshi la akiba kwa vijana 150 wa wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani wakiwa makini kufuatilia hotuba za viongozi ambazo zilikuwa zinatolewa wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo yaliyofanyika leo Agosti 6,2020.(PICHA ZOTE NA SAID MWISHEHE-MICHUZI TV)

======  ======  ======

Na Said Mwishehe, Michuzi TV 

WAKATI Watanzania wakielekea katika Uchaguzi Mkuu unaotarajia kufanyika Oktoba 28,2020,Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani imesema haitovumilia wala haiko tayari kujaribiwa. 

Hivyo imewataka wananchi wote kwa ujumla kuwa sehemu ya kuhakikisha Wilaya hiyo inakuwa salama wakati wote kwani bila ya amani hakuna maendeleo, hivyo ni wajibu wa kila mwananchi kuifanya Kisarawe inakuwa salama wakati wote. 

Hayo yamesemwa leo Agosti 6,2020 na Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe Jokate Mwegelo wakati akifungua mafunzo ya jeshi la akiba(mgambo) kwa vijana 150 wa wilaya hiyo ambayo yatafanyika kwa kipindi cha miezi minne. 

Jokate Mwegelo amesema wananchi wote wanafahamu nchi inaelekea kwenye uchaguzi mkuu , hivyo ni kipindi ambacho Wilaya hiyo kupitia Kamati ya ulinzi na usalama imejipanga vema kwa ajili ya kufanikisha uchaguzi unafanyika kwa amani na utulivu. 

"Nimekuja kufungua mafunzo haya ya jeshi la akiba , nikiamini tunakwenda kuanda vijana wazalendo kwa nchi yetu, vijana watakaokuwa tayari kuhakikisha hawashiriki kwenye matukio ya uvunjifu wa amani.Kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu huwa kuna vitendo vingi vinavyoashiria kuvura amani. 

"Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Kisarawe yote iko hapa, na kwa niaba yao naomba nieleze wazi, tumejipanga, hatutakuwa tayari kujaribiwa na mtu yoyote.Hivyo ni ombi langu kwenu ninyi vijana pamoja na vijana wengine wote wa Kisarawe na wananchi kwa ujumla tuwe wamoja kwa kuifanya Kisarawe yetu kuendelelea kubaki salama,"amesema Jokate. 

Amesisitiza kuwa hawatacheka na mtu yoyote atakayefanya vurugu amani."Kipindi hiki cha uchaguzi, ni kipindi muhimu na sisi tuko vizuri na yoyote atakayejihusisha na vurugu au uvunjifu wa amani hatamvumiliwa." 

Ameomba vijana hao wanaopatiwa mafunzo hayo kuwa sehemu ya raia wema ambao wataisaidia wilaya hiyo kuwa salama na kubwa zaidi wawe sehemu ya watoa taarifa ambazo zitasaidia kudhibiti matukio ya uvunjifu wa amani na uhalifu. 

Pia amesema watakapokuwa wakirejea majumbani wakawe sehemu ya kutoa elimu kwa jamii kuhusiana na kujiepusha na vitendo visivyovumulika. 

Mkuu wa Wilaya hiyo pia ametumia nafasi hiyo kueleza ni vema vijana wakahakikisha wanashiriki kikamilifu kuchagua viongozi wao kuanzia ngazi ya diwani, mbunge na Rais na hivyo kila mmoja atunze kitambulisho chake cha kupigia kura."Ni haki ya kila mwananchi kushiriki kwenye kuchagua viongozi wao kwani hiyo ni haki yao kwa mujibu wa Katiba." 

Kuhusu mafunzo hayo Mkuu wa wilaya Jokate amesema wanapaswa kuwa watiifu na na raia wema kwa kuhakikisha wanalinda rasilimali za Taifa na kwamba Taifa linawategemea huku akisisitiza ni imani yake baada ya mafunzo hayo watakuwa mfano wa kuigwa kwa jamii. 

Kuhusu utimamu wa mwili Jokate amewataka vijana hao kujiepusha na mambo ambayo yatawafanya kuzorotesha miiili yao na ni vema wakazigatia afya zao kwa kujiepusha na ngono zembe, uvutaji wa dawa za kulevya na uzembe. 

Kwa upande wake Mshauri la Akiba Wilaya ya Kisarawe Meja Mohamed Wawa amesema mafunzo hayo yalianza Julai 13 na yatarajiwa kumalizika Novemba 2 mwaka huu."Jumla ya vijana 150 wanaendelea na mafunzo haya , kati ya hao wasichana ni 62 na waliobakia ni wavulana".



APP YETU MPYA: Sasa unaweza kusoma kwa urahisi kupitia APP yetu. Download hapa kwa KUBOFYA HAPA

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini