*Zimo za bweni 26 kwa kila mkoa na za kutwa 1, 000 kwenye kata 718
*Aelezea mfumo wa ukuzaji ujuzi kwa vijana, ujenzi wa skimu za umwagiliaji
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali itajenga shule mpya 1,026 ambapo kati ya hizo, shule 26 zitakuwa za bweni zenye uwezo wa kupokea wanafunzi kati ya 1,000 hadi 1,500 kwa kila mkoa na zitajengwa kwa awamu tatu.
Ametoa kauli hiyo leo (Jumamosi, Februari 13, 2021) katika hotuba yake aliyoitoa wakati wa kuahirisha mkutano wa pili wa Bunge jijini Dodoma. Bunge limeahirishwa hadi Machi 30, mwaka huu.
Waziri Mkuu amesema shule nyingine mpya 1,000 za kutwa zenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 400 kwa kila shule, zitajengwa chini ya mradi wa maboresho ya elimu ya sekondari yaani Secondary Education Quality Improvement Programme (SEQUIP) ambao utatekelezwa kwa muda wa miaka mitano (2020/2021 - 2025/2026).
Amesema Benki ya Dunia iliidhinisha mkopo wa kiasi cha dola za Marekani milioni 500 sawa na sh. trilioni 1.2 kwa ajili ya mradi huo, na kwamba ukikamilika, utakuwa ni mwarobaini kwa changamoto ya miundombinu ya shule za sekondari.
“Shule hizo zitajengwa kwenye kata 718 zisizo na sekondari za kata na kwenye maeneo yaliyoelemewa na idadi kubwa ya wanafunzi. Hivyo basi, nitumie nafasi hii kuwaelekeza viongozi na watendaji wa Serikali za Mitaa wasimamie kikamilifu utekelezaji wa mradi huu ili kufikia malengo yaliyokusudiwa,” amesisitiza.
Wakati huohuo, akielezea suala la ukuzaji ujuzi miongoni mwa vijana, Waziri Mkuu amesema katika kipindi cha Julai, 2020 hadi Januari, 2021 vijana 10,178 wamepatiwa mafunzo na kutathminiwa ujuzi walioupata nje ya mfumo rasmi wa mafunzo nchi nzima ambapo vijana 9,736 wamefaulu na kupatiwa vyeti na Mamlaka ya Mafunzo na Ufundi Stadi (VETA).
Amesema vyeti hivyo vinawawezesha vijana hao kutambulika, kujiendeleza kiujuzi, kujiajiri pamoja na kupata kazi katika taasisi na kampuni mbalimbali. “Vijana hao ni wenye ujuzi katika fani za uashi, useremala, ushonaji, ufundi bomba, uchomeleaji na uungaji vyuma, ufundi magari, ufundi umeme, ukarabati wa bodi za magari, upishi na uhudumu katika hoteli. Aidha, vijana 36 wamegharamiwa na Serikali kwa ajili ya kuhudhuria mafunzo ya kilimo cha kisasa nchini Israel,” amesema.
“Katika nusu ya pili ya mwaka 2020/2021, vijana wapatao 4,616 watapatiwa mafunzo na kurasimishwa ujuzi walionao kupitia mfumo huu. Aidha, Januari 2021, vijana 1,203 wa vyuo vya elimu ya juu na kati wamehitimu mafunzo ya uzoefu wa kazi kupitia kampuni mbalimbali kulingana na fani walizosomea, na wahitimu 2,037 wamewezeshwa na wanaendelea kupata mafunzo ya uzoefu wa kazi katika taasisi binafsi na za umma ambayo yatachukua muda wa kipindi cha mwaka mmoja.”
Amesema wahitimu 2,421 wanaandaliwa ili waanze mafunzo Machi, 2021 katika fani za ushonaji nguo, useremala, uashi, uchorongaji vipuri, ufundi magari, umeme, bomba, terazo, upishi, na utoaji huduma za mahoteli, utengenezaji wa simu, majokofu, viyoyozi, upakaji rangi, uandishi wa alama, utengenezaji wa umeme wa magari, utengenezaji wa nywele na utanashati, uchoraji, n.k.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ameeleza mikakati ya Serikali ya kuimarisha kilimo cha umwagiliaji nchini ambapo amesema katika kipindi cha mwaka 2015 hadi 2020, Serikali imefanikiwa kujenga na kukarabati skimu za umwagiliaji 179 ambazo zimeongeza eneo la umwagiliaji kutoka hekta 461,000 mwaka 2015 hadi hekta 694,715 mwaka 2020 sawa na ongezeko la asilimia 50.7.
“Hii ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango Kabambe wa Taifa wa Umwagiliaji wa mwaka 2018 yaani Revised National Irrigation Master Plan (RNIMP 2018) ambao umeainisha hekta milioni 29.4 zinazofaa kwa kilimo cha umwagiliaji,” amesema.
Aidha, Waziri Mkuu amesema Serikali imekamilisha ujenzi wa maghala 14 ya kuhifadhia mavuno katika skimu za umwagiliaji za Ngana na Makwale (Kyela), Magozi na Tungamalenga (Iringa), Mbuyuni-Kimani, Ipatagwa, Kongolo-Mswiswi na Motombaya (Mbarali), Lekitatu (Arusha), Mombo (Tanga), Uturo (Mbeya), Bagamoyo (Pwani), Mkindo na Mkula (Morogoro).
“Katika hatua ya kuongeza mnyororo wa thamani kwenye uzalishaji wa mazao ya kilimo, kati ya maghala hayo, maghala sita yamewekewa na vinu vya kukobolea mpunga,” ameongeza.
APP YETU MPYA: Sasa unaweza kusoma kwa urahisi kupitia APP yetu. Download hapa kwa KUBOFYA HAPA
0 Comments