Katika kuadhimisha Siku ya Mazingira Duniani, Ubalozi wa Marekani wasaidia ujenzi wa vyoo rafiki wa mazingira Shule ya Msingi Karume , wilayani Temeke. | ZamotoHabari.


Ubalozi wa Marekani, kupitia Mfuko wa Balozi wa Kusaidia Miradi ya Kijamii, umefadhili ujenzi wa vyoo vilivyo rafiki wa mazingira vilivyojengwa kwa matofali maalumu rafiki wa mazingira (eco-bricks) katika Shule ya Msingi Karume wilayani Temeke. 

Uzinduzi rasmi wa vyoo hivi uliofanywa jana na Balozi Donald Wright na Afisa Elimu wa Wilaya ya Temeke Rashid Ally, unakwenda sambamba na maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani, ambayo huadhimishwa kimataifa tarehe 5 Juni.

Vyoo hivyo vimejengwa kwa kutumia ruzuku ya Dola za Kimarekani 7,000 kutoka katika Mfuko wa Balozi wa Kusaidia Miradi ya Kijamii, mfuko unaoendeshwa na Ubalozi wa Marekani kusaidia miradi midogo midogo inayolenga kuisaidia na kuihimiza jamii kujitegemea. Ruzuku hii ilitolewa kwa asasi isiyo ya kiserikali itwayo PHEDES, inayoongozwa na mkurugenzi John Ambrose na meneja mradi Hellen Sailas.

Helen ni mjasiriamali wa mazingira ambaye amebuni mbinu ya kutengeneza matofali kwa kuyayusha takataka za plastiki zilizookotwa katika fukwe za Dar es Salaam. Kutokana na ruzuku kutoka katika Mfuko wa Balozi, hivi sasa Hellen ameweza kuanzisha kampuni yake, Arena Recycling Industry ili kuzalisha matofali zaidi.

Akizungumza katika hafla hiyo, Balozi Wright alisema, jitihada za kulinda mazingira zinaweza pia kuzalisha fursa mpya. “ Ninaipongeza jamii na PHEDES kwa ubunifu na wazo la kutatua matatizo mawili kwa wakati mmoja – yaani tatizo la uchafuzi wa bahari kutokana na takataka za plastiki na lile la kukosekana mfumo wa maji na usafi. Nimefurahishwa pia na maono ya HelIen ya kusafisha fukwe za Tanzania na kutumia takataka za plastiki zilizokusanywa kutoka katika fukwe hizo kutengeneza matofali yaliyotumika kujengea vyoo vipya hapa Shule ya Msingi Karume. Kupitia mradi huu sote tumechangia kuondoa takataka za plastiki wakati huo huo tukitatua mahitaji ya jamii.”

Aidha, Balozi alisema kuwa mradi huu unadhihirisha dhamira ya dhati ya Serikali ya Marekani kusaidia elimu nchini Tanzania.

“Shule zinapokuwa salama, safi na zenye vifaa vyote vinavyohitajika wanafunzi hujifunza vyema zaidi. Kutokana na vyoo hivi, wanafunzi wa shule hii watajielekeza zaidi katika masomo yao. Hii ni mojawapo kati ya miradi midogo ambayo Serikali ya Marekani inawekeza katika siku zijazo za Tanzania kwa kupanua fursa za kielimu kwa vijana wake.

Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, Serikali ya Marekani imewekeza Dola za Kimarekani milioni 67.1 katika mfumo wa elimu ya msingi wa Tanzania kwa kusaidia kuandaliwa kwa mtaala unaozingatia umri kufundisha kuandika, kusoma na kuhesabu kwa darasa la kwanza hadi la nne, hivyo kuwafikia wanafunzi 825,000 na takriban walimu 10,000 katika wilaya 42 nchini. Aidha, Serikali ya Marekani imesaidia kwa kutoa vifaa vya kufundishia na kujifunzia na kusaidia shughuli mbalimbali za kuishirikisha jamii.”
Balozi wa Marekani nchini Dkt Donald Wright akipata maelezo kutoka kwa Mkurugenzi wa Arena Recycling Industry Bi. Helena Silas kuhusu matofali ya mfano yaliyotengenezwa kwa kutumia taka za plastiki ambayo ni rafiki wa Mazingira, yaliyotumika kujengea vyoo katika Shule ya Msingi Karume wilayani Temeke jijini Dar es Salaam. (Picha kwa Hisani ya Ubalozi wa Marekani).



APP YETU MPYA: Sasa unaweza kusoma kwa urahisi kupitia APP yetu. Download hapa kwa KUBOFYA HAPA

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini