Na Bakari Madjeshi, Michuzi TV
MCHEZAJI wa Kimataifa wa Ghana, Bernard Morrison ameomba msamaha Mashabiki wa Yanga SC kwa kitendo cha kuondoka Klabuni hapo, miaka miwili iliyopita na kuhamia kwa Watani wa Jadi Simba SC, uhamisho ulioleta utata kwenye mkataba.
Morrison ameomba radhi mbele ya Mashabiki lukuki wa timu hiyo na Uongozi wa Klabu hiyo wakati akitambulishwa katika tamasha la Siku ya Mwananchi kwenye dimba la Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, Agosti 6, 2022.
“Naomba msamaha kwa Mashabiki wote wa Yanga S.C. kwa miaka miwili iliyopita kuondoka klabuni hapa, najua hamkufurahi lakini nimerudi na nawaomba msamaha, bado naipenda Yanga S.C.”, amesema Morrison.
“Miaka miwili iliyopita, niliwahi kupanda kwenye jukwaa hili nilisema nipo kwenye Chuo Kikuu cha Soka la Tanzania na kwa sasa kwenye Klabu ya Yanga nipo kwenye ‘level’ nyingine ya Shahada ya Pili (Master’s Degree)”, amesema Morrison.
Pia, Morrison amesema wanaamini kufanya vizuri msimu ujao kutetea mataji yote matatu ambayo wametwaa msimu uliopita, mataji ya Ligi Kuu Soka Tanzania Bara, Michuano ya ASFC, na Ngao ya Hisani.
Morrison amesema, “Kwa sasa Yanga S.C. imekuwa kubwa sana imesajili Wachezaji wazuri wenye viwango na kuna Kocha Mkuu, Nasreddine Nabi ambaye amefanikisha yote msimu uliopita akishirikiana na Benchi lake la Ufundi”.
Kwenye tamasha hilo, Msemaji wa Klabu hiyo, Haji Sunday Manara amefanya ‘surprise’ kwenye tamasha hilo la Wananchi baada ya kudai kufika kama ‘MC’ aliyealikwa kwenye shughuli hiyo ambayo imehudhuriwa na idadi kubwa ya Mashabiki.
“Mimi nimekuja kama walivyokuja kina Maulid Kitenge, Zembwela na Dacota, mimi nimealikwa tu kama ‘MC’ na nikitoka hapa naenda kwenye shughuli huko Kigogo, ahsanteni sana Wananchi”, amedai Manara.
Tembelea Website ya Nyimbo za Injili Africa. Pakua na Kusikiliza bure bila malipoBOFYA HAPA
0 Comments